Utangulizi
Maisha na
mafanikio ni vitu viwili tofauti lakini vinavyoenda sambamba siku zote. Kila
mwanadamu anatamani afikie malengo fulani ambayo anajiwekea katika maisha yake.
Malengo hayo huwa hayafanani kwa watu wote hivyo mafanikio ni tofauti kwa watu
tofauti. Kwamfano mwanafunzi anaweza akapanga kufikia maadhimio Fulani katika
masomo yake na mwingine akapanga kupata zaidi kulingana na anavyoona uwezo
wake. Anapofikia malengo aliyojiwekea, hii inamaanisha kwamba amefanikiwa. Lakini
unaweza kujikuta mara nyingi umepanga mipango mingi lakini haufanikishi hata
mpango mmoja kati ya mipango hiyo uliyoipanga. Swali ni je, ulifuatisha kanuni
za kufanikiwa? Ulijiandaa kufikia malengo uliyojipangia? Kanuni zifuatatazo
zinaweza kukusaidia kufika sehemu katika mipango yako kama kweli utatilia
maanani.
1.
Fanya kazi kwa
bidii.
Watu wengi
tumekuwa tukifanya kazi kama kutimiza ratiba tu za kila siku na wengine
tunafanya kazi tu kwakuwa mwisho wa mwezi tutapata mshahara. Na wengine
tunafanya kazi ilikusudi tusionekane tunashinda tu nyumbani na kuanza kuitwa
yale majina ya “goli kipa” na mengine mengi. Lakini katika kufanya kazi hizo
tunakuwa hatuweki juhudi na kuzifanya kwa bidii matokeo yake tunakosa ufanisi
na umakini katika kazi hizo tunazozifanya.
Wengine
wanashindwa kuweka bidii katika kufanya kazi walizonazo kwasababu tu
walilazimishwa labda na wazazi wao kuchukua fani fulani walipokuwa wanajiunga
na elimu ya juu. Hivyo kufanya kazi ambazo hawazipendi, hivyo wanajikuta
wanafanya tu ilimradi siku iende lakini hawazipendi. Je, unawezekana kuweka
bidii katika kitu ambacho haupendi? Jibu sahihi hapa itakuwa ni hapana. Kufanya
kazi kwa bidii kunahitaji utayari wa kufanya kitu kutoka moyoni. Mtu akishindwa
kufanya kazi kwa bidii itakuwa ni vigumu sana kufikia malengo aliyojipangia
katika maisha na mtu kama huyo asahau kabisa maendeleo katika maisha yake.
2.
Ishi kulingana na
kipato chako.
Watu wengi
wanapenda kuishi maisha ambayo ni ya juu kuliko kipato chao walichonacho au
wanachoingiza kila mwezi. Hivyo kila mwisho wa mwezi unajikuta unapokea
mshahara au hesabu zako zote za mwezi zinaishia kulipa madeni hakuna faida.
Tatizo ni nini hasa? Ulijaribu kuishi maisha ambayo si maisha yako. Kama
ungekuwa unaishi maisha ambayo hakika ni ya kwako basi ungetulia na
kukipangilia kile kipato chako unachopata kwa mwezi na kutosha. Kwamfano
unagawa mshahara wako au kipato chako kwa mwezi na matumizi yako na kuhakikisha
kwamba kipato kinatosha na unapata akiba. Unaweza ukaainisha matumizi yako kwa
mwezi, ukagawanya kwa kutumia asilimia na ukapata mgawanyo wa hela yako au
kipato chako.
3.
Usiige namna ya
kuishi.
Kila mtu ana
namna yake ya kuishi kwahiyo hakuna mtu hata mmoja atakuwa sawa na mwenzake
hata ukijilazimisha kufanana na mtu mwingine haiwezekani kwani hata mapacha wa
kufanana hawawezi kuwa na maisha sawa au mafanikio sawa katika maisha. Katika
maisha ya uanafunzi kila mtu anatamani angekuwa wa kwanza lakini kinachotokea
ni kwamba hata kama wanafunzi wote watapata alama sawa darasani wa kwanza hadi
wa mwisho ataonekana tu. Malengo tuliyonayo yanatofautiana kutoka mtu mmoja na
mwingine kwahiyo unapojaribu tu kuishi maisha ya mtu mwingine unajikuta
unapoteza mwelekeo na malengo yako hivo kushindwa kufikia mafanikio katika kile
ulichopania kufikia kwa kipindi fulani.
Ukiishi maisha
yako utaweza kuwa na msimamo wa kile unachopanga kufanikisha katika masiha.
Hautakuwa tayari kubadilishwa mtazamo wako na mtu yeyote kwasababu utakuwa
unajua kitu unachofanya, utakuwa na mtazamo chanya kuelekea mafanikio yako.
4.
Fanya kitu
ambacho unaweza si kama vile watu watakavyo.
Mara nyingi
katika maisha tumejikuta tumefanya vitu ili kuwafurahisha watu wengine na si
kwasababu tunauwezo wa kufanya vitu hivyo. Wewe mwenyewe ndiye unajua mapungufu
au udhaifu wako na uwezo wako wa kufanya jambo fulani. Kwahiyo kusikiliza sauti
za wengine mara nyingi hupelekea kufanya kitu ambacho wewe hauwezi. Kwa mfano
unaweza kuwa ni daktari mzuri lakini mwongeaji; kwasababu ya hali yako ya
uchangamfu na kuongea na watu vizuri, kuwa na lugha ya ushawishi basi watu
wanakushauri wewe uwe mwanasiasa. Kumbuka si kila mtu mwongeaji basi
anawezakuwa mwanasiasa na siyo kila mtu mkimya anaweza kuwa daktari.
Kusikiliza
ushauri wa watu wengine ni jambo zuri na la msingi sana, lakini kufanya vile
wanavyotaka wengine ni jambo la hatari sana katika maisha. Kumbuka wewe
mwenyewe ndiye unayejijua ulivyo na hakuna mtu mwingine anayekujua wewe. Sisi
watu wengine tunachokiona ni matokeo ya maamzi yako wewe. Hivyo kukujua wewe ni
pale tu unapofanya maamzi yako.
Mfano mzuri ni
kwenye mpira wa miguu, kama wewe ni mfungaji hauwezi kulazimishwa na watu
ukakae golini. Kufungwa utafungwa tu kwasababu unatenda kazi katika nafasi
ambayo siyo ya kwako bali unatakakutimiza tu wanayotaka watu unaowasikiliza.
Wewe mwenyewe unajua kuwa kudaka hauwezi kabisa lakini unakaa kwasababu tu
umewasikiliza watu wanasemaje. Kama unafanya mambo yako ili kiiridhisha jamii
au watu wanaokuzunguka, sahau mafanikio.
5.
Epuka starehe.
Starehe ni moja
kati ya changamoto kubwa sana katika kufanya watu wasiendelee, hii hupelekea
watu kutumia pesa zao vibaya. Si pesa tu bali hata kupoteza muda mwingi ambao
kama ungetumika kwa kufanya mambo ya msingi ungevuka hatua moja katika maisha
yako. Starehe siku zote inahitaji pesa na muda, ukiwa kwenye starehe huko
unakutana na ushindani mkubwa wa watu wanaotumia pesa, wewe pamoja na kutokuwa
na pesa za kutosha za mengineyo, utajikuta unatumia pesa hadi za akiba na
mwisho wa siku unaambulia madeni yasiyokoma.
Mfano mzuri ni
kuingia kwa simu za kisasa (Androids, Smart Phones, Tablets, nk) kumepelekea
vijana wengi (kwa ulimbukeni) kuzinunua na kujiunga kila mtandao wa kijamii.
Siyo vibaya lakini matumizi yake yamekuwa kinyume na kumfanya kijana kushindwa
kufanya kazi kwa ufanisi huku akichati mambo yasiyofaa na kutumia pesa nyingi
sana katika kununua kifurushi vya mtandao “Internet”
6.
Uwe na nidhamu ya
pesa.
Kila mtu
anahangaika kuitafuta pesa kila iitwapo leo. Wakati pesa hiyohiyo ikiwa ngumu
kwa watu fulani fulani kwa wengine siyo shida kubwa kwani wanaweza kuipata
kiurahisi. Wakati wengine wakidharauliwa kwa kutokuwa na pesa wengine
wanaheshimiwa na kuabudiwa kwakuwa nazo hizo pesa. Lakini kitu cha muhimu sana
katika pesa ni “NIDHAMU YA PESA”
Pesa siyo mbaya
lakini maamzi anayoyatoa mtumiaji wake huwa ni mabaya sana. Hivyo pesa hizohizo
zimekuwa laana kwa baadhi ya watu na kwa wengine zimekuwa Baraka. Kinachofanya
kwa wengine iwe Baraka na wengine iwe laana ni matumizi yake. Kukosa nidhamu ya
pesa na kuitumia ovyoovyo hupelekea mtu kujenga uadui na watu wengine na
kujitenga kabisa mbali na Mungu. Katika kufikia mafanikio lazima tuwe na
nidhamu katika kuzitumia pesa.
7.
Fikiri juu ya
maisha ya baadaye.
Wahenga walisema
“fikiri kabla ya kutenda” na katika maisha pia mtu anashauriwa kuwa na picha
kichwa ya aina ya maisha ambayo anataka kuja kuishi. Lazima kila jambo
unalofikiria na kulifanya liwe na malengo fulani katika maisha yako. Kabla ya
kufanya maamzi ya suala lolote lile unatakiwa uwe na mipango ya nini unataka
kufanya na unataka kuishi maisha ya aina gani hapo baadae. Je, una tamani ukiwa
mzee wajukuu wako wajifunze nini kutoka kwako? Unataka jamii inayokuzunguka
isemeje kuhusu wewe? Je, unata uje kudharaurika au kuheshimika?
Matokeo ya
kufikiria kwako ndiyo yatakayokupa picha halisi ya maisha ambayo utakuja
kuishi. Kufikiria vibaya siku zote humpelekea mtu kuishi maisha mabaya na
matokeo ya kufikiria vizuri siku zote hupelekea maisha mazuri.
8.
Angalia watu
unaoandamana nao.
Siku zote wale
unaoandamana nao utakuwa kama wao. Hauwezi hata siku moja ukajadili mambo ya
msingi wa watu wapuuzi. Siku zote uandamane na watu waliofanikiwa katika eneo
ambalo unafanyia kazi. Inawezekana ni ofisini au biashara, kilimo na shughuli
nyingine. Watu waliofanikiwa (siyo wote, bali wale wenye mtazamo chanya
kuelekea wengine) si kila mtu aliyefanikiwa basi atataka na wewe ufanikiwe kwa
jamii nyingi za kiafrika kwani wengi wanatamani wafanikiwe peke yao.
Usijifanyie urafiki na mtu mpaka pale utakapokuwa umezisoma njia zake.
Siku zote
ukiandamana na watu walioshindwa watakuwa wanakukatisha tamaa na watakufanya
usiendelee mbele. Marafiki unaojifanyia siku zote wanatakiwa wawe na mawazo na
mtazamo chanya. Lazima wasiwe watu wa kukata tamaa bali wawe na msaada kwako
hata kimawazo.
No comments:
Write comments